Monday, October 31, 2016

Wazazi pamoja na watoto 476 kufundishwa biashara



Mama mjamzito

WASICHANA 476 mwenye umri kuanzia miaka 11 hadi kufikia 17 waliokuwa katika masomo shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Morogoro na kupata mimba na kushindwa kuendelea na masomo, wamejitokeza kujisajili na Shirika lisilo la kiserikali la Young Strong Mothers Foundation (YSMF) ili kupata usaidizi wa fursa za kielimu katika biashara na ujasiriamali.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Jackie Bomboma, ameyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili baada ya kikao cha majaribio ya mfumo wa ufuatiliaji na tathimini ya shughuli za maendeleo na ustawi wa jamii kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bigwa, Manispaa ya Morogoro.
Bomboma amesema idadi hiyo imepatikana tangu Julai mwaka jana hadi mwaka huu, na kueleza kuwa watoto wengi wa kike walishindwa kumaliza elimu ya masomo yao kuanzia darasa la saba na sekondari na waliokuwa wakisubiri matokeo ya mitihani yao.
Amesema kundi hilo lilijikuta likipata mimba zisizotarajiwa zinazochangiwa na vishawishi kutokana na mazingira duni ya vipato katika familia wanazotoka.
Kwa mujibu wa Bomboma, alianzisha shirika hilo la kuwasaidia wasichana waliopata mimba za utotoni wakiwa shuleni ama wakati wakusubiri matokeo ya mitihani yao na kujifungua watoto .
“Kwa sasa shirika limesajili wasichana 476 ambao wanapatiwa fursa za elimu ya biashara na ujasiriamali na wengine 15 wanasoma masomo ya ufundi katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Bigwa,” alisema na kufafanua kuwa wasichana hao wanatoka katika kata 11 za Manispaa ya Morogoro ambao baadhi yao ni watoto waliokuwa darasa la sita na wenye umri kuanzia miaka 11.
Alilitaja kundi jingine lilioathiriwa kutokana na mimba za utotoni ni la wanafunzi waliohitimu darasa la saba na wakisubiri matokeo ya mitihani yao na wanaosubiria matokeo ya kidato cha nne.
“Katika mahojiano wakati wa usajili wao, wengi wamepata mimba za utotoni wakiwa darasa la sita na umri wao ni kati ya miaka 11 na 12, wapo wanaosubiri matokeo ya darasa la saba na kwa sekondari ni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu na idadi ndogo kwa wanaosubiria matokeo ya kidato cha nne,” alieleza Bomboma.
Hata hivyo, alisema kila mmoja amekuwa akitoa sababu zake na iliyo kuu ni umaskini wa kipato katika kaya wanazoishi jambo ambalo linawafanya watoto hao wa kike kujitumbukiza kwenye vishawishi na kwenda nje kupata huduma ya kujisaidia wao na wakati mwingine familia wanazotoka.

Na hadija abdallah 
chanzo: Habari leo

No comments:

Post a Comment